TOPIC 4: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Fasihi andishi ni tawi la
fasihi linalotumia sanaa ya maneno kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya
maandishi. Zipo aina nyingi za fasihi andishi, miongoni mwa hizo ni pamoja na
hadithi fupi, riwaya, tamthiliya na mashairi.
Maana ya Uhakiki
Dhana ya Uhakiki
Uhakiki
ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi
fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Hii ina maana kwamba uhakiki wa
kazi za fasihi hautoki katika ombwe, kuna kanuni na taratibu mbalimbali
zinazoongoza kufanya uhakiki, na hii ndio sababu kuna nadharia kadha wa kadha
za uhakiki wa kazi za kifaishi. AU kwa lugha rahisi tunaweza kusema, uhakiki ni
uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kama vile riwaya, tamthiliya na mashairi
kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui.
Misingi ya Uhakiki
Kwa
ujumla mhakiki wa kazi za fasihi anapofanya uhakiki wa kazi za kifasihi, huwa
analenga vipengele viwili. Pengine analenga kuhakiki fani ya kazi husika au maudhui ya kazi hiyo na wakati mwingine vyote
viwili. Kwa hiyo kupitia vipengele hivi ndipo atachambua vitu vingi kama vile
ujumbe, falsafa, matumizi ya lugha, dhamira, mandhari na kadhalika.
Kuhakiki
Fani
Katika
utunzi wa kazi za kifasihi, Fani hutumika kama nyezo ya kuwasilisha mawazo ya
mwandishi kwa njia ya kisanaa zaidi. Fani ni mbinu anayoitumia mwandshi ili
kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia.
Vipengele
vya fani ni pamoja na wahusika, mandhari, lugha,
muundo na mtindo.
Mtindo
Mtindo
ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii mmoja na
mwingine. Kwa mfano, namna msanii anavyotumia lugha, anavyoteua msamiati, namna
anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi ya kwanza, ya pili au ya
tatu). Kwa mfano katika riwaya ya “Barua Ndefu kama hii” iliyoandikwa na
Mariama Ba ametumia mtindo wa barua ya kirafiki kuanzia mwanzo hadi mwisho, hii
pia inaonesha mtindo wake wa kipekee.
Muundo
Muundo
ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi yake.
mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi, kwa upande wa visa na mtukio.
Kuna
aina mbili za kupangilia matukio
§
Msago, hii ni namna ya moja kwa
moja ya kusimulia matukio, yaani kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa
namna yalivyotukia. Huu ni muundo wa moja kwa moja.
§ Urejeshi,
huu ni usimuliaji wa kurukaruka hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia
katikati, akaja mwisho na kumalizia na mwanzo
Wahusika
Wahusika
ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufanikisha ujumbe
kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa wahusika katika
makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Wahusika
wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa kazi ya fasihi.
Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza sehemu mbalimbali katika kazi
ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa kitabu hadi mwishoni mwa kitabu.
Wahusika hawa wawe ni wakuu au wadogo wanaweza kugawanyika katika makundi yafuatayo:
Mhusika mviringo ni mhusika ambaye anabadilika kitabia na kimawazo kulingana na hali halisi ya maisha. Kwa mfano wanaweza kuanza kama watu wema lakini hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wabaya au wanaweza kuanza kama watu wabaya na hali ya maisha ikawabadilisha na kuwa watu wema.
Mhusika bapa ni mhusika ambaye habadiliki kulingana na hali halisi ya maisha. Mfano; kama ni mwema basi atakuwa mwema kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho na kama ni mbaya basi atakuwa mbaya kuanzia mwanzo wa hadithi hadi mwisho.
Mhusika shinda yuko katikikati ya mhusika papa na mviringo. Huongozwa na matendo ya hao wahusika wawili. Hajitokezi na msimamo wake imara.
Mandhari
Mandhari
hii ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza
kuwa halisi kama vile baharini, njiani, msituni, kijijini, mijini au ya
kufikirika kama vile kuzimu, mbinguni, peponi n.k.
Lugha
Lugha
ndio nyenzo kubwa ya msanii katika kazi za fasihi, miongoni mwa vipengele vya
lugha ni tamathali za semi pamoja na semi.
Fani za Lugha
Tanakali za Sauti:Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika.
Tashbiha: Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’, ‘ja’. mfano, Mwembamba kama sindano.
Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Mfano, "Sungura aliposhindwa, akasema sizitaki hizi mbichi".
Takriri: Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Mfano, alikimbia, alikimbia, alikimbia hadi akashika nafasi ya kwanza.
Ukinzani: Ukinzani ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana.
Sitiari: Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo ‘ni’ ama ‘kuwa’. Mfano; Maisha ni mlima, juma ni mwamba.
Taswira: Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
Taashira: Ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa.
Jazanda: Ni kulinganisha vitu viwili moja kwa moja bila kutumia viunganishi.Mfano Bwana Juma alioa kasuku.
Majazi: Majazi ni pale tabia za wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.
Lakabu: Ni mbinu ya mhusika kupewa/kubandikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa zake.
Chuku: Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu, kutilia Chumvi.
Semi
Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:
Nahau ni usemi unaotumia maneno ya kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyotofauti na maana ya kawaida ya maneno hayo. Nahau huwa na vitenzi.
Misemo ni semi fupifupi ambazo hutumiwa mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. Misemo haina vitenzi.
Maswali ya Balagha: Tashititi au maswali ya balagha ni maswali yanayoulizwa na msimulizi au mhusika ambayo hayahitaji jibu.
Uzungumzi Nafsiya: Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote.
Ritifaa: Mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe.
Kuchanganya Ndimi: Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili. Mfano, "alisimama kwanza kwa muda, before he went aliniambia nisimwambie mtu yeyote yule, you know!"
Kuhamisha Ndimi: Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu. Mfano: Kazi hii ni ngumu sana, sitaweza kuifanya. People are trying to convince me to stay here but I think I can't, I must go!
Methali: Methali ni misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa. Mhusika, mwandishi wa fasihi anaweza kutumia methali kupitisha ujumbe.
Mbinu nyingine za Kisanaa
Kinaya ni mambo katika sanaa kuwa kinyume na matarajio ya hadhira.
Kejeli ni mbinu ya sanaa inayotumia maneno kudharau au kukemea kitendo au mtu fulani.
Taharuki ni mbinu ya kusimulia au kuandika riwaya/hadithi kwa kufanya hadhira na/au wahusika wajawe na hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye; hamu ya kutaka kuendelea kusoma/kusikiliza. Baadhi ya hadithi huishia kwa taharuki na kuilazimisha hadhira yake ijikamilishie au ibaki ikijiuliza maswali.
Sadfa ni kugongana kwa vitendo viwili vinavyohusiana kana kwamba vilikuwa vimepangwa, japo havikuwa vimepangiwa.
Kisengere Nyuma, Mwandishi ‘hurudi nyuma’ na kuanza kusimulia kisa kilichokuwa kimetendeka kabla ya alichokuwa akisimulia. Aidha, mwandishi hubadilisha wakati wa masimulizi na kuwa wakati wa kisa hicho. Hutumika sana kuonyesha mhusika anapokumbuka kitu, au kutupatia msingi wa jinsi mambo yalivyoanza.
Kisengere Mbele, Mwandishi anapobadilisha wakati na kusimulia mambo yatakavyokuwa siku za usoni; au kutumia lugha isiyo moja kwa moja kutabiri yatakayojiri. Utabiri.
Kuhakiki Maudhui
Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.
Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
Migogoro; hii ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.
Msimamo; katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Kwa mfano, katika tamthilia ya “Pesa zako zinanuka” mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwani amejadili matatizo yanayochangia kukwama kwa ujenzi wa jamii mpya.
Falsafa ni mawazo ya busara yenye kutawaliwa na misingi mahususi juu ya asili na maana ya ulimwengu na maisha ya mwanadamu. Ni msimamo wa msanii katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii. Falsafa ya mwandishi inaweza kujulikana kwa kusoma kazi zake zaidi ya moja.
Mtazamo ni hisia au uelewa wa mwandishi juu ya jambo fulani. Kwa mfano anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kidini, au anaweza kutazama jambo fulani kwa mtazamo wa kisiasa au kisayansi.
Mafunzo; ni mawazo ya kuelimisha yanayopatikana katika dhamira mbalimbali za kazi ya fasihi.
Kufaulu na Kutofaulu kwa
mwandishi
Kufaulu
au kutofaulu kwa mwandishi kunategemea jinsi alivyoweka uwiano mzuri kati ya
fani na maudhui kwa namna ambavyo inaleta uhalisia. Mfano, endapo msanii
atakuwa na mhusika Mkongo lakini akawa anazungumza kiswahili kilichojaa misemo
na nahau alafu kimenyooka kama mtu wa pwani itakuwa vigumu kusema amefaulu
kwani hakuna uwiano mzuri kati ya mhusika mwenyewe na lugha anayoitumia.
Kiswahili cha Kongo ni tofauti kabisa na kiswahili kinachozungumzwa na watu wa
pwani (Tanzania).